Chama cha upinzani cha UDP kupitia mwenyekiti wake taifa John Mwamose Cheyo kimewapongeza wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusimama pamoja kuhakikisha miswada ya sheria iliyofikishwa bungeni kuhusu mali asili za nchi inapitishwa kwa maslahi ya taifa bila kuangalia tofauti ya itikadi zao.
Aidha chama hicho kimekiri kuwa muda uliotolewa wa kupitia miswada hiyo ulikuwa mdogo, jambo ambalo wamedai hakuna wa kulaumiwa kutokana na udharura wa jambo lenyewe kutokana na taarifa zilozotolewa na tume mbili zilizoundwa na rais.
Akiongea na vyombo vya habari kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa chama hicho taifa John Cheyo amesema mikataba iliyoingia nchi kuhusu mali asili mbalimbali za nchi ikiwamo madini ilikuwa ni ya kuinyonya nchi, na yeye wakati akiwa mbunge alikuwa akilisemea hilo mara kwa mara, na hata kwenye kamati ya jaji Mark Bomani ambayo yeye alikuwa mjumbe na kwamba kilichokosekana kwa wakati huo ni kiongozi mwenye uthubutu wa kuchukua hatua pale anapoona nchi inaibiwa.
Hata hivyo Bwana Cheyo amesema moja ya changamoto ambayo inaikumba serikali ya tanzania ni utekelezaji wa sheria zilizopo, hivyo ameomba pindi miswada hiyo itakaposainiwa na kuwa sheria, usimamizi wake uwe madhubuti kwa manufaa ya watanzania wote.
Wakati huo huo Bwana Cheyo amewataka viongozi wastaafu ambao bado wanaendelea kuhudumiwa na serikali kuhakikisha wanatumia muda wao mwingi kujenga umoja wa watanzania, na kwamba kunahaja ya nchi kuwa na sheria inayoelekeza haki na wajibu wa wastaafu hao.
No comments:
Post a Comment