Friday, July 7, 2017

Viwango vipya vya mishahara Zanzibar, Wawekezaji waishauri serikali kuangalia upya

SHEINWawekezaji katika Sekta ya Utalii Zanzibar wameishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuangalia upya viwango vya mishahara vilivyopendekezwa kwa kima cha chini kwa upande wa sekta binafsi cha shilingi 300,000 ili kuepusha hatua za kupunguzwa kwa wafanyakazi kwa vile wengi wao watashindwa kumudu kulipa viwango hivyo vipya vya mishahara.
Ushauri huo wameutoa katika mapendekezo yaliyofikiwa katika Mkutano wa pamoja ulioitishwa na Jumuiya ya Wawekezaji wa Sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI) kujadili mapendekezo ya mishahara yaliyotolewa na Waziri mwenye dhamana wa Kazi Zanzibar Modeline Castico ya kutaka watumishi wa sekta binafsi walipwe mishahara ya kima cha chini kutoka shilingi 145,000 hadi 300,000 kwa mwezi.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa ZATI Seif Miskry amesema wanatambua kuwa gharama za maisha zimepanda lakini kama viwango hivyo vitatekelezwa bila ya kuangaliwa upya wawekezaji katika sekta hiyo watalazimika kupunguza idadi ya wafanyakazi kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji wa miradi yao.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano huo wamesema kimsingi hivi sasa kuna wafanyakazi katika sekta hiyo tayari wananufaika na kiwango hicho cha mishahara na mabadiliko yaliyotolewa na Serikali yatawalazimisha kupitia upya mishahara yao jambo ambalo litahatarisha ajira za wafanyakazi wengi.
Sekta ya Utalii visiwani Zanzibar ndio nguzo kuu ya uchumi inayochangia asilimia 27 ya pato la taifa na asilimia 83 ya fedha za kigeni, pamoja na kutoa ajira kwa watu 22,000 na kunufaisha wazalishaji katika sekta ya kilimo, uvuvi, mifugo na biashara.

No comments:

Post a Comment

most viwed news

Uhuru na Lowassa waomba Wakenya kuvumiliana

Aliyekuwa waziri mkuu nchini Tanzania na mgombea wa urais katika chama cha upinzani Chadema katika uchaguzi uliopita Edward Lowassa amewata...